Thursday, May 31, 2018

UKUSANYAJI WA MAPATO KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAONGEZEKA HADI KUFIKIA ASILIMIA 16

Na Veronica Kazimoto,Zanzibar 

Wastani wa ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha miezi 10 ya Mwaka wa Fedha 2017/18 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umeongezeka hadi kufikia asilimia 16 ukilinganisha na asilimia 14 katika kipindi kama hicho cha 2016/17. 

Hayo yamesemwa na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere baada ya kumaliza Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambacho TRA ilikuwa mwenyeji.

"Katika kikao hiki tulichomaliza leo, tumejadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafanikio tuliyoyapata ambayo ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato katika Jumuiya yetu kutoka asilimia 14 kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17 hadi kufikia asilimia16 katika kipindi kama hicho cha Mwaka huu wa Fedha wa 2017/18", alisema Kichere. 

Kichere alieleza kuwa, pamoja na mafanikio hayo, kikao hicho kimejadili na kukubaliana masuala mbalimbali yakiwemo kuimarisha utozaji kodi kwa watu binafsi na wafanyabiashara wadogo na kuweka mipango mahususi ya kutoza kodi stahiki kutoka kwa wafanyabiashara hao. 

"Pia, tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kupeana taarifa na kuonyeshana mianya ya ukwepaji kodi ili kudhibiti na kukomesha hali hiyo," alibainisha Kichere.

Makubaliano mengine ni pamoja na kuweka mikakati mahususi ya kushughulikia masuala ya uadilifu kwa kuwa, Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki kama ilivyo kwenye taasisi nyingine za Serikali ndani ya Jumuiya, kumekuwa na changamoto hiyo ya uadilifu. Hivyo, Makamishna Wakuu hao wamekubaliana kuongeza ufanisi katika kukagua mwenendo wa maisha wa watumishi wa Mamlaka zao ikiwa ni pamoja na kuwashitaki wale wote ambao si waadilifu kama sehemu ya kupambana na rushwa. 

"Ndugu waandishi wa habari, pamoja na kupambana na rushwa, tumekubaliana pia kupunguza gharama za mifumo ya TEHAMA kwa kuwajengea uwezo watumishi wa ndani ya Mamlaka ili kupunguza gharama ambazo zinatumika kuwalipa watalaam kutoka katika mataifa mengine," aliongeza Kichere.

Kwa upande wa Makamishna Wakuu wa Jumuia hiyo ya Afrika Mashariki, wakizungumza kila mmoja kwa wakati wake, wote wamekubali kuzingatia makubaliano hayo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ndani ya nchi zao.

Kabla ya mkutano huo, Makamishna Wakuu hao wa taasisi za kodi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki walikutana na Wawakilishi wa Shirika la Misaada la nchini Japan (JICA) kutathmin miradi wanayofadhili kwa lengo la uboreshaji shughuli za forodha ndani ya Jumuiya. 

Katika mkutano huo, Shirika la JICA lilipongezwa kwa kurahisisha uondoshaji wa mizigo na kuhudumia abiria wanaosafiri kupitia mipaka ya nchi za Jumuiya hiyo kutoka saa 8 za awali hadi saa 2 na nusu kwa sasa hususani katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Rusumo ambacho kilijengwa kwa msaada wa JICA.

Kituo hicho ni moja kati ya vituo 7 vya Huduma za Pamoja Mipakani vilivyojengwa kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa Maendeleo. Sambamba na pongezi hizo, Shirika hilo limeombwa kusaidia ufadhili wa uunganishaji mifumo ya TEHAMA na uwezeshaji wa mawakala wa forodha ili kupata ufanisi zaidi.

Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu hao, kimehudhuliwa na watendaji wapato 80 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), Mamlaka ya Mapato Rwanda (RRA), Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR), Mamlaka ya Mapato ya Jamhuri ya Sudani Kusini pamoja na Mwakilishi kutoka Sekritariat ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kikao kijacho kinatarajia kufanyika mwezi Novemba, 2018 nchini Kenya.


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji. Kushoto ni Mhe. Audace Niyonzima wa Mamlaka ya Mapato Burundi na kulia ni Bi. Doris Akol, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA).

 Mwenyekiti wa Kamati ya Watalaam wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mahariki Bi. Martine Nibasumba kutoka Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR) akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo kwa Makamishna Wakuu (hawapo pichani) wakati wa Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji.


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna Wakuu wenzake na baadhi ya wajumbe wa Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji.

WALIOKAIDI KUHAMA KWENYE MAENEO YENYE MAFURIKO SAME SASA KUKAMATWA

Eneo la Kitongoji cha Mferejini lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kuanzisha kambi kwa ajili ya Wahanga wa Mafuriko .
Wahanga wa Mafuriko wakianza ujenzi wa nyumba za Miti kwa ajili ya kujisitiri katika eneo la Ruvu Mferejini.

Makazi ya wananchi hawa kwa sasa wanalala nje ,wakiteseka na Baridi,Mbu na wanyama wakali kama Nyoka hali ambayo inatishia Afya zao.
Hata hivyo tayari serikali imeanza kufikisha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo ya Maji kwa ajili ya kunywa pamoja na kupikia.

Na hizi ndio sehemu za makazi ya wananchi hawa.

Huduma Muhimu kama Choo zimeanza kujengwa katika eneo hilo.
Wananchi Jamii ya Massai pia ni miongoni mwa waathirika wa Mafuriko hayo.

Mkuu wa wilaya ya Same,Rosemery Senyamule akiwa ameongozana na Katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro,Mhandisi Aisha Amour wakitembelea moja ya Kaya ya Jamii ya Wafugaji walioanza maisha mapya katika maeneo yaliyotengwa na Serikali.

Baadhi ya Nyumba za Jamii ya Kimasai zikianza kujengwa katika eneo hilo.
Kama ilivyo ada kwa tamaduni za Mila za jamii ya Maasai kina mama ndio watendaji wakubwa wa shughuli za Nyumbani kiwemo ujenzi wa Nyumba kama anavyoonekana Bibi huyu.
Arikadharika shughuli ya uchotji wa maji vivyo hivyo.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.

SERIKALI imetoa siku mbili kwa wananchi waliosalia katika Vijiji vya Ruvu Mferejini na Ruvu Marwa wilayani Same ,Mkoani Kilimanjaro vilivyozingirwa na maji kuondoka mara moja na kwamba watakao kaidi wataondolewa kwa kutumia nguvu na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Zaidi ya watu wapatao 2000 wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya kufikwa mafuriko kutokana na mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha huku eneo lililoathirika zaidi na mvua hizo ni ukanda wa tambarare wa wilaya ya Same unaopakana na Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Licha ya Idadi hiyo ya watu kuyahama makazi yao lakini bado wapo waliokaidi kuondokana na hapa Serikali kupitia Mkuu wa wilaya ya Same ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya hiyo ,Rosemerry Senyamule ,ikatoa agizo.

Serikali imetenga maeneo kando ya milima iliyopo katika kitongoji cha Mferejini kwa ajili ya Kambi za Muda kwa watu waliokosa Makazi ,Clouds Habari imefika katika Kambi hizo na kujionea maisha mapya ya wahanga wa mafuriko huku misaada ya kibinadamu ikihitajika zaidi .

Licha ya kukosekana kwa baadhi ya huduma katika eneo hili bado wananchi hawa wanahitaji msaada wa hali na mali ili angalau kuweza kunusuru Maisha yao kutokana na Baridi kali ,Mbu na hata wanyama wakali wakiwemo Nyoka.

Katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi ,Aisha Amour ni miongoni mwa baadhi ya viongozi waliowatembelea wahanga wa mafuriko kwa ajili ya kutoa pole .

Mafuriko katika vijiji hivi yanatajwa kuwa hutokea kila baada ya Miaka 10 na kwamba mara ya mwisho yalitokea mwaka 2008 huku chanzo kikitajwa kuwa ni kujaa kwa Bwawa la Nyumba ya Mungu ambapo ujazo ulifikia Mita za ujazo 689.88 ambazo kwa sasa zimeanza kupungua hadi kufikia mita za ujazo 689.80 baada ya maji kuanza kuelekea kwenye maeneo ya makazi kwa kupitia mto Pangani.

KATIBU TAWALA MKOA WA KILIMANJARO,MHANDISI AISHA AMOUR AONGOZA WAJUMBE WA KAMATI YA MAAFA KUTEMBELEA BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU

Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro,Mhandisi Aisha Amour akiwa ameongozana na wajumbe wengine wa Kamati ya Maafa kutembelea Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo wilayani Mwanga ambalo linatajwa ujazo wake wa maji wa kawaida umepitiliza na kusababisha Mafuriko kwa wakazi waishio kando ya Bonde la Mto Pangani.

Mhandisi ,Aisha Amour akitizama kina cha Maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kilichofikia Mita za ujazo 689.88 . 
Sehemu ya Bwawa la Nyumba ya Mungu. 


Baadhi ya wakazi wa vijiji vya jirani na Bwawa la Nyumba ya Mungu wakitumia usafiri wa Mitumbwi kusafiri kutoka upande mmoja kwenda upande wa Pili. 
Sehemu ya Mapitio ya Maji baada ya kujaa katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ,maji haya yanaelekea katika maeneo ambayo yapo makazi na mashamba ya watu yaliyopo pembezoni mwa Bonde la Mto ,Pangani. 

Maji yakiendelea kuenea katika uwanda wa Tambarare baada ya kujaa Bwawa la Nyumba ya Mungu. Na Dixon Busagaga wa Gobu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.

Wednesday, May 30, 2018

MNYETI AAGIZA MANYARA IKAMILISHE VIWANDA 100

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, wakiwemo maofisa tarafa, madiwani, watendaji wa kata, vijiji, walimu na wenyeviti wa vijiji, juu ya kufanya kazi kwa uadilifu na kutumikia jamii, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Mhandisi Raymond Mushi akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga juu ya kufanya kazi na kuwahusia kuwa siku mbili ambazo mtu hawezi kufanya chochote ni jana na kesho hivyo waitumie siku ya leo kwa kutimiza wajibu wao, kulia ni Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Nicodemus Tarmo.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Vijijini Mkoani Manyara, Vrajilal Jituson, akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yao ikiwemo suala la elimu.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Esta Mahawe akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambapo alijitoa mashuka 10 kwa ajili ya wagonjwa watakaotumia kwenye zahanati ya kijiji hicho iliyozinduliwa na Mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameziagiza Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha zinatekeleza agizo la uanzishwaji wa viwanda 100 na hadi mwezi Septemba mwaka huu viwe vimekamilika. 

Mnyeti akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, alisema kila halmashauri ya mkoa huo wenye halmashauri saba, inapaswa iwe na viwanda 15. Mnyeti alisema serikali ilitoa agizo la kila mkoa uanzishe viwanda 100 hivyo na mkoa wa Manyara nao unapaswa kuhakikisha unatekeleza agizo hilo kwa kila halmashauri kuwa na viwanda 15. 

Alisema agizo hilo linatakiwa kutekelezwa kwa kila sekta ikiwemo kilimo na mifugo ambazo ndizo shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi wengi wa mkoa huo. “Watumishi wa umma wanapaswa kutambua kila taaluma waliyoisomea wanapaswa kuwekeza kwenye fikra ya viwanda kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa sekta hiyo,” alisema Mnyeti. 

Aliwapongeza mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hamis Malinga kwa kutekeleza agizo hilo la uanzishwaji wa viwanda vipya. “Kwenye miezi mitatu iliyopita Halmashauri ya Babati mlikuwa mmeshafanikisha uanzishwaji wa viwanda nane na hadi kufikia mwezi Septemba mtakuwa mmekamilisha viwanda 15 hongereni sana,” alisema Mnyeti. Mkuu wa wilaya ya Babati, mhandisi Raymond Mushi alisema wananchi wa eneo hilo ni wachapakazi wazuri na hujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.

Mushi alisema kwa kiasi kikubwa wananchi wa wilaya yake ni wachapakazi huku wakishirikiana na serikali katika kufanikisha maendeleo mbalimbali.Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jitu Son alisema wameshajipanga kutekeleza hilo kupitia viwanda mbalimbali vilivyopo jimboni humo. Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Hamis Malinga alisema kwa kiasi kikubwa wamefanikisha utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.“Kwenye suala la migogoro ya ardhi, kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mwenyekiti wake mheshimiwa mkuu wa wilaya kwa kiasi kikubwa imefanikisha kusuluhisha japo kuwa maeneo machache yaliyobaki na yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.

Jituson alisema kwenye eneo hilo kuna viwanda mbalimbali vipya vilivyojengwa vikiwemo vya mafuta, sukari, kukoboa mpunga, unga, na kiwanda cha vyakula vya mifugo. Alisema kupitia nafasi ya vijiji vingine 30 kupatiwa umeme wa Rea awamu ya tatu, itasaidia kuanzisha viwanda vidogo na vya kati kwa wajasiriamali mbalimbali waliopo kwenye jimbo hilo. 

Mkazi wa Kijiji cha Endanachang’ John Lorry alisema serikali na sekta binafsi zinapaswa kujipanga na kuanzisha kiwanda cha biskuti ili zao la mbaazi lipate soko. Lorry alisema changamoto ya soko la mbaazi imekuwa kero kwa jamii ila kupitia viwanda wakulima wengi wa eneo hilo wataweza kunufaika kwa kupata sehemu ya uhakika ya kuuza zao hilo.

RAS SHINYANGA AFUNGUA MAFUNZO KWA KAMATI YA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela amefungua mafunzo kwa wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Shinyanga yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kupiga vita ukatili katika jamii.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza leo Jumatano Mei 30,2018 yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga yamekutanisha wadau mbalimbali wanaohusika katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Investing in Children and their Societies (ICS – Africa). 

Awali akizungumza,Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga Glory Mbia alisema lengo la mafunzo hayo ni kupata maoni na mapendekezo mbalimbali katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. “Lengo la mafunzo haya ni kupata uelewa wa pamoja na kutengeneza mkakati namna gani tunafanya katika kutokomeza vitendo vya kikatili katika mkoa”,alisema Mbia. 

Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo alisema mkoa wa Shinyanga bado una tatizo kubwa la ukatili dhidi ya watoto na wanawake hivyo zinahitajika nguvu za pamoja 

“Tunamshukuru mwenyezi Mungu mauaji dhidi ya albino yamebaki historia katika mkoa wetu,lakini katika jamii kumekuwa na unyanyasaji hasa wa watoto,kupitia kamati hii naamini kwa pamoja kama tutaamua kwenda pamoja hatua kwa hatua tutaweza kutokomeza vitendo vya ukatili katika mkoa huu”,alieleza Msovela. “Akina mama na watoto wengi wameathirika kisaikolojia,kimwili,wapo watoto wamekosa elimu kutokana na unyanyasaji wanaopitia kwa pamoja naamini sheria ambazo zipo na umoja huu tutaweza kukabiliana na ukatili wanaofanyiwa wanawake na watoto”,alisema. 

“Kwa namna ya pekee niwashukuru sana wadau wetu wa maendeleo ICS ambao wamejitolea kudhamini mafunzo haya,na hivi sasa kamati imeshaundwa kutoka katika ngazi ya kata,halmashauri na sasa tunaendelea na mafunzo kwa ngazi ya mkoa”,aliongeza Msovela. 

Kwa upande wake,Afisa Maendeleo Mwandamizi, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mathias Haule alisema umaskini umekuwa chanzo cha vitendo ukatili dhidi ya wanawake hivyo ili kutokomeza vitendo hivyo ni vyema wanawake wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi huku wadau wote wakiweka nguvu pamoja katika kuwalinda na kuwatetea wanawake na watoto. 

Naye Meneja wa shirika la ICS nchini,Kudely Sokoine Joram alisema ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,shirika hilo limekuwa likishirikiana na serikali ili kuhakikisha wanawake na watoto wanakuwa salama katika jamii. 

“Kupitia mradi wetu wa masuala ya ulinzi na usalama wa watoto tunafanya mradi huu katika manispaa ya Shinyanga,Shinyanga Vijijini na wilaya ya Kishapu na baada ya serikali kumaliza kutengeneza mwongozo,ilituomba tunapokuwa na rasilimali basi tuweze kusaidia serikali kuhakikisha kamati zinaundwa na zinapata mafunzo ndiyo maana hata haya mafunzo tumeyawezesha sisi”,alieleza. 

Meneja huyo wa ICS alisema katika ngazi ya halmashauri,kata na vijiji mpaka sasa wamezisaidia kamati 25 wakishirikiana na serikali na wanaendelea kuwezesha uundwaji wa kamati ili kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 

“Sisi kama wadau wa maendeleo tunashughulika na masuala ya malezi na matunzo bora ya watoto,masuala ya ulinzi wa watoto kwa mfano miongozo ya serikali na sheria zilizopo lakini pia kuwezesha familia katika masuala ya kiuchumi,kujenga uwezo wa taasisi ndogo ndogo na maeneo husika yanayoshughulika na maendeleo ya jamii”,alisema Joram. 
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akifungua mafunzo ya kujengea uwezo kwa wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Shinyanga leo Mei 30,2018 - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akifungua mafunzo na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga Glory Mbia akielezea malengo ya mafunzo hayo ambapo alisema lengoni kupata maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu namna ya kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga. 
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Meneja wa shirika la ICS nchini Tanzania, Kudely Sokoine Joram akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambapo alisema wameamua kufadhili mafunzo hayo ili kushirikiana na serikali katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Meneja wa shirika la ICS nchini Tanzania, Kudely Sokoine Joram akizungumza ukumbini.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon akielezea namna wanavyoshiriki katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga.


Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Afisa Maendeleo Mwandamizi, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mathias Haule akielezea Muhtasari kuhusu Mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada ukumbini.
Mafunzo yanaendelea.

Kushoto ni Afisa Maendeleo Mwandamizi, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mathias Haule na Afisa Mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kutoka shirika la ICS mkoa wa Shinyanga,Shadia Nurdin wakiangalia nyaraka zinahusu masuala ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

SERIKALI YAAGIZA WAMACHINGA WATENGEWE MAENEO YA KUFANYIA BIASHARA

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiongea na wamachinga wakati  wa kufungua  Mkutano Mkuu wa Shirika la umoja wa wamachinga Tanzania- SHIUMA leo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiongea na wamachinga wakati  wa kufungua  Mkutano Mkuu wa Shirika la umoja wa wamachinga Tanzania- SHIUMA leo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma, Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo  akiongea na baadhi ya viongozi wa shirika la umoja wa wamachinga Tanzania – SHIUMA leo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma, Jijini Dodoma.

Na Angela Msimbira,

Wakuu wa Wilaya wameagizwa kuzisimamia halmashauri nchini kuhakikisha kuwa zinatenga maeneo maalum ya kufanyia biashara ndogondogo (machinga) ili  waweze kuendesha shughuli zao bila kuvunja sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali. 


Agizo hilo limetolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemeni Jafo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirika la umoja wa wamachinga Tanzania – SHIUMA uliofanyika leo katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya Dodoma, Jijini Dodoma.



Alisema Wakuu wa Wilaya wana wajibu wa kuratibu na kuhakikisha kuwa maeneo ya kufanyia bishara kwa wamachinga yanatengwa na Halmashauri ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa utaratibu bila kuvunja sheria za nchi. 



Aliongeza kuwa wamachinga ni watu muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania kwa kuwa wafanyabiashara wadogo ndio wanaoleta muunganiko wa watu katika kada mbalimbali wakiwemo wasomi wenye shahada, astashaada, kidato cha sita, kidato cha nne, darasa la saba na wasiosoma kabisa wote huunganika na kufanyabiashara kama wamachinga.



Alisema kati ya watanzania milioni 50, walioajiriwa serikalini na sekta ya umma ni 520,000, hivyo kundi kubwa ni la watu ambao ama wamejiajiri au wameajiriwa katika sekta binafsi. 



“Lakini kundi kubwa ni wale watu wanaojishughulisha kwa kutafuta riziki zao wenyewe ambao watu hao ndio unapata asilimia kubwa wako katika kundi la wamachinga,” alisema Mhe.Jafo na kuongeza:



“Utakuta mtu anafanyabishara katika mazingira magumu ambayo yanamfanya kila wakati kutokuwa na uhakika wa kupata kipato cha siku jambo ambalo linaathiri familia yake na kuongeza umaskini nchini, hivyo ifike mahali wakuu wa Wilaya waweke mikakati ya kuhakikisha wamachinga wote wanapatiwa maeneo bora ya kufanyia biashara ili wajikwamue kiuchumi,  “alisisitiza Waziri 



Aliongeza kuwa Serikali imejiwekea mkakati wa kutengeneza masoko mazuri na ya kisasa kwa kuweza kuweka mazingira bora kwa wamachinga kufanya biashara zao katika maeneo stahiki.



Aidha Waziri Jafo alisema kuwa Viongozi wanatakiwa kutafakari na kutatua kero ya maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara wamachinga, hivyo serikali imeanza mpango mkakati  wa ujenzi wa masoko mazuri ya kisasa ili wafanyabishara waweze kufanya kazi katika mazingira bora na tayari imetenga shilingi bilioni 149 kwa ajili ya ujenzi wa masoko, stendi za kisasa na viwanda vidogo.



 “Nimetoa maagizo soko lolote litakalojengwa lazima mustakabali wa wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwepo awali umejulikana na kuwa kipaumbele kwa kupatiwa maeneo ya kufanyia biashara pindi majengo hayo yanapokamilika hivyo viongozi wa halmashauri wahakikishe wanatoa kipaumbele kwa wafanyabiashara waliokuwepo awali,” alisema Jafo.



Alisema kuwa Serikali imekuwa ikiwekeza katika miradi mikubwa ikidhani inawagusa maskini lakini kwa bahati mbaya masoko mengi yanayojengwa wanaonufaika ni watu wenye fedha na kuwaacha wafanyabiashara waliokuwepo awali kabla soko kujengwa. 



Hivyo nawaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wananchi masikini wanapatiwa nafasi katika masoko hayo ili waweze kujiongezea kipato.Amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri wote nchini kuhakikisha kuwa kabla soko halijaanza kujengwa kufanyike tathmini ya wafanyabishara waliokuwepo awali ili wawe kipaumbele pale soko linapokamilika.






Wakati huohuo Mhe. Jafo amewataka wamachinga nchini kuhakikisha wanajiunga na bima iliyoboreshwa ili iwawezeshe kuwasaidia pale wanapokuwa wagonjwa wao na familia zao kwa kuwa afya ni uhai.

MBUNGE RITTA KABATI ATOA SADAKA YA TENDE KWA WAUMINI WA DINI YA KIISLAM MANISPAA YA IRINGA


Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM)  Ritta Kabati akiongea na viongozi wa misikiti yote ya manispaa ya Iringa wakati wa utoaji sadaka ya tende kwa waumini wa dini ya kiislamu wa manispaa ya Iringa kwa ajili ya kuadhimisha mfungo wa ramadhan kwa waislamu wa wote wa manispaa ya Iringa. 
Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza amemshukuru mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kutoa sadaka ya tunda la tende kwa waiislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza akikabidhi tende alizokabidhiwa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kutoa sadaka kwa waiislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan.
Mkuu wa walimu na msimamizi wa misikiti ya Dhinureyn Tanzania Abdul Salam Ahmad Ayub akimshukuru mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa sadaka aliyoitoa kwa waislam katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan.
Baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) na viongozi wa misiki ya  manispaa ya Iringa walipohudhulia zoezi la utoaji wa sadaka ya tende ilitolewa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati



NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati ametoa sadaka ya tende kwa waumini wa dini ya kiislamu wa manispaa ya Iringa kwa ajili ya kuadhimisha mfungo wa ramadhan kwa waislamu wa wote wa manispaa ya Iringa

Akizungumza wakati wa kukabidhi sadaka hiyo katika msikiti wa Dhinureyn Gangilonga Kabati alisema kuwa kila mwaka amekuwa akifutulisha katika maeneo mbalimbali hivyo mwaka huu ameamua kununua tende na kugawa kwenye misikiti yote ya manispaa ya Iringa.

“Unajua mwaka huu tende ni tunda ambalo linahitajika katika kipindi hiki cha mfungo na kuna watu ambao hawana uwezo wa kununua tende hizi na ukiangalia mwaka huu tende zimepanda bei sana hivyo kwa kiasa ambacho nakipata nimeamua kutoa sadaka hii kwa waumini wa kiislam” alisema Kabati

Kabati aliwataka wananchi wengine kuendelea kumuabudu mwenyezi mungu pale ambapo tunapata nafasi ili kupunguza maovu ambayo tumekuwa tukiyatenda kwa kukusudia au bila kukusudia na kufanya hivyo basi mwenyezi mungu atatuongezea pale ambapo tumepunguza kwa ajili ya kumtumiaka mungu.

“Katika kipindi hiki nawaomba wazazi,walezi na viongozi wetu naomba tutoe elimu kwa vijana wetu kwa kuwapa elimu ya dini pamoja maadili ya nchi yetu kwa lengo la kuwajenga vijana wawe wanamcha mungu hasa kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan” alisema Kabati

Kabati alisema kuwa ametoa sadaka ya tende tani mbili ambayo ipo katika halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa ajili ya misikiti yote na vituo vya watoto yatima ambavyo vinawatoto wa kiislam ambao wanafunga katika kipindi hiki cha mfungo.

“Mimi nimeleta tani mbili ili kuongezea nguvu wafungaji wa kipindi hiki lakini kutoa sadaka kwa mwenyezi mungu katika kipindi ambacho waislamu wapo kwenye mfungo wa ramadhan nakuwasidia wale ambao hawana uwezo wa kununua tunda hili la tende” alisema Kabati

Kwa upande wake mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza amemshukuru mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kutoa sadaka ya tunda la tende kwa waiislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan.

“Tunashukuru sana kwa sadaka hii ambayo umetusaidia kwa waislam wa manispaa ya Iringa kwa msaada wako ambao utasiadia kwa wale ambao wanamahitaji maalumu na mungu atakuongezea aple ulipopunguza na mungu akubariki” alisema Masenza.Masenza aliwaomba maimamu kuwagawia tende hizo waislam ambao hawana uwezo wa kununua tende tukani ili nao wapate hiki chakula cha kwanza pindi unapofungua na wale wenye uwezo wa kununua tende dukani basi waendelee kununua

Naye mkuu wa walimu na msimamizi wa misikiti ya Dhinureyn Tanzania Abdul Salam Ahmad Ayub alisema kuwa msaada aliotoa mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati utawasaidia waislam waliofunga.“Sadaka hii aliyoitua huyu mbunge Kabati umekuja wakati muafaka na umamanufaa makubwa sana kwa waislam kwa kuwa tumehimizwa kufuturu kwanza tende hivyo kwa muislam kula tende ni fadhila kubwa sana”alisema Ayub

Ayub alisema kuwa katika kipindi hiki cha mfungo waislam tunatakiwa kupeana vyakula ili kila mtu ambaye hana kitu aweze kupata chakula na ndio alivyofanya huyu mbunge Ritta Kabati kwa waislam wa manispaa ya Iringa.

“Zamani watu walikuwa wanatandika jamvi nje wakati wa kufutulu ili waweze kufutulu na waislam ambao hawana uwezo na ndio uzalendo wenyewe huo,hivyo tunamuombea mbunge huyu aendelee na moyo huo huo” alisema Ayub