Friday, March 31, 2017

Watumishi Wa OSHA Wapewa Changamoto

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, akiwahutubia wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kikao chao cha baraza. Kulia ni Kaimu  Mtendaji Mkuu wa Wakala Bi. Khadija Mwenda na viongozi wa baraza hilo. 

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mara baada ya kufungua kikao chao cha baraza.) 
Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi (hayupo pichani) alipofungua kikao cha baraza lao mjini Dodoma jana.


Mabadiliko ya mazingira ya ufanyaji biashara yanayoletwa na maendeleo ya uchumi wa viwanda pamoja na mnyororo wa thamani, yameelezwa kuwa changamoto kubwa katika jitihada za kuimarisha hali ya usalama na afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi hapa nchini.

Changamoto hiyo imetolewa na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Bw, Eric Shitindi, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mjini Dodoma leo.

Amesema mabadiliko hayo yanahusisha matumizi ya teknolojia za kisasa na ongezeko kubwa la idadi ya wafanyakazi katika sekta zote za umma na za binafsi jambo ambalo linahitaji utaalamu mkubwa katika kuweka na kusimamia mifumo ya kulinda afya na kuwahakikishia usalama wafanyakazi wote wanapokuwa katika sehemu zao za kazi.

“Hivyo mkiwa kama wataalamu katika masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi mnatakiwa kuwa na mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto hizo. Hii itakuwa ni pamoja na kubadilika kifikra na kimtazamo katika utendaji kazi,” alisema Katibu mkuu Shitindi.

Katibu mkuu huyo amesisitiza muhimu wa kutafuta mbinu mbadala ya kuweza kupanua wigo wa kufanya kazi hasa kwa kuzingatia ukubwa wa kazi zilizopo.

Aidha Bw. Shitindi ameupongeza OSHA kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango kazi wake katika kipindi cha robo tatu za mwaka huu wa fedha (2016/2017) ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika baraza hilo, taasisi imevuka malengo katika kaguzi, utoaji wa mafunzo ya usalama na afya kazini pamoja na huduma mbali mbali zitolewazo mahali pa kazi.

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu aliahidi kuendelea kuisaidia OSHA kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za kiutendaji na kuwaasa watumishi wa Wakala kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuepuka kujihusisha na vitendo vya upokeaji rushwa wanapotekeleza majukumu yao.

“Wizara imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya namna mnavyohudumia wateja na kushuka kwa maadili ya kiutendaji miongoni mwa watumishi, mfano masuala ya rushwa, hivyo wakati tunaendelea kushughulikia matatizo hayo ni vyema sasa mkaanza kubadilika kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali ya utendaji kazi katika taasisi,” amesisitiza Bw, Shitindi.

Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi wa OSHA ambacho kimeanza leo kitamalizika kesho ambapo pamoja na mambo mengine kitapitia na kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha wa (2017/2018) ili kujiridhisha kama itawawezesha kufanikisha utekelezaji wa malengo ya wakala yaliyowekwa

No comments: