Friday, March 31, 2017

KAMATI YA KUKABILIANA NA KIPINDUPINDU YAKUTANA KUANDAA MPANGO MKAKATI WA MWAKA MMOJA


Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afaya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla akieleza mipango iliyoandaliwa ya kukabiliana na maradhi ya kipindupindu iwapo yatatokezea katika kikao kilichofanyika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo chekundu Mjini Zanzibar.
Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Mazingira Rukaiya Mohamed Said akiwasilisha taarifa ya kikao kilichopita cha Kamati hiyo kilichofanyika mwezi uliopita.
Afisa kutoka Jumuia ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Zanzibar Jokha Masoud Salim akitoa mchango wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Kamati ya kukabiliana na kipindupindu wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu.
Afisa uperesheni na huduma za kibinadamu, Kamisheni ya kukabiliana na maafa Makame Khatibu Makame akitoa mada juu ya mpango wa kukabiliana na maafa Zanzibar katika cha Kamati hiyo kilichofanyika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.



Na Khadija Khamis –Maelezo

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt Fadhil Moh’d Abdalla ameitaka jamii kubadili tabia kwa kuweka mazingira yaliyowazunguka safi na kuhakikisha wanatumia maji safi na salama ili kujiepusha na maradhi ya mribuko .

hayo ameyasema wakati wa kikao cha kamati ya kitaifa ya kuandaa mpango mkakati wa kudhibiti maradhi ya kipindupindu hasa kipindi hichi ambacho mvua za masika zimeanza kunyesha.

Alisema lengo kuu la kamati hiyo ni kufanya tadhmini ya muendelezo wa mpango kazi wa kudhibiti maambukizi ikiwemo kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii na kupambana na mazingira hatarishi katika maeneo mbali mbali ya Manispaa ya Zanzibar.

Ameishauri Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha maji yanayotumiwa na wananchi yapo katika hali ya safi na salama kwa kutia dawa vianzio vyote vya maji na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kufanya uharibifu kwenye njia za maji kwa kutoboa mabomba yanayosamba maji .

Alieleza changamoto zinazowakabili kwa sasa ni kuwepo kwa wafanyabiashara wasiofuata taratibu za usafi wa chakula na mazingira katika utendaji mzima wa biashara zao.

Alisema uzoefu unaonyesha maradhi ya kipindupindu mara nyingi hutokea wakati wa kipindi cha mvua hivyo tahadhari zinahitajika katika kuweka mazingira katika hali ya usafi

“Wananchi wahakikishe wanakunywa maji ya kuchemsha au kuyatia watergard ili kuweka tahadhari wakati huu wa kipindi cha mvua za masika kwani kunauwezekano mkubwa wa kuchafuka vyanzio vya maji kwa kuingia maji machafu,” Alisema Mkurugenzi kinga .

Aliwashauri wananchi wanaoishi sehemu za mabondeni kuchukue juhudi za makusudi kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka majanga katika kipindi hichi cha mvua za masika

No comments: