Tuesday, June 30, 2015

MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA BENKI YA POSTA TANZANIA (KUFUTA NA KUWEKA MASHARTI YA MPITO), 2015 (THE TANZANIA POSTAL BANK {REPEAL AND TRANSITIONAL PROVISION} ACT, 2015)

 (Yanatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya kanuni za Bunge,Toleo la mwaka 2013)
Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu,Subhanahu wa Taala kwa kutujalia sote afya njema na kuendelea na kazi ya kulitumikia Taifa.
Pili nishukuru Chama changu cha CUF kwa uamuzi wake wa busara wa kunirejesha mimi kuwa Mgombea wa Jimbo la Mkanyageni na kama ukataji wa majimbo utaathiri Jimbo hilo, naamini chama pia kitafanya uamuzi wa hekima na busara kwa faida ya Chama wala sio matakwa binafsi ya yoyote.
Tatu nichukue nafasi hii kumpongeza Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif kwa ukomavu, uvumilivu na uhodari wake kisiasa na hata kama walimzuia kuingia katika Baraza, yeye alikwishafanya uamuzi mapema zaidi wa kutokwenda katika Baraza hilo maana hakuwa tayari kwenda kinyume na wajumbe wa Baraza kutoka CUF wakiwemo mawaziri. Uamuzi huo alioufanya mapema zaidi kuungana na Wawakilishi wake ndicho kilichomfanya Spika wa Baraza na wajumbe wa CCM kukasirika na kuchukua uamuzi wa chuki na kisasi ambao kwa waliokuwa hawajui wanadhani kuwa yeye alikuwa na shauku ya kwenda Barazani humo.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha CUF cha kususia baraza ni cha demokrasia popote pale Duniani kinachoonesha kutokukubaliana na jambo kwa njia ya kistaarabu. Kwa kuwa uchaguzi huru ni mchakato na unaanzia katika daftari la kuandikisha wapigakura, hivyo basi kitendo chochote cha kuwazuia au kutokuwaandikisha wapiga kura iwe Bara au Zanzibar ni jambo la hatari la kukiuka Demokrasia na kuufanya uchaguzi usiwe huru na wa haki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaisihi,kuionya na kuitaka Serikali iwaandikishe watu wote wenye sifa katika daftari la wapiga kura kwa Bara au Zanzibar ili kufikisha makisio ya wapigakura milioni 24. Aidha
Haitakuwa uchaguzi huru na haki ikiwa idadi kubwa ya wapiga kura imeachwa kuandikishwa na kukoseshwa haki yao ya kikatiba.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa ni kwamba hali ya siasa Zanzibar imeshavurugwa na ilianzia pale vikosi vya ulinzi vilivyopewa silaha kuwapiga wananchi katika zoezi la kujiandikisha. Baya zaidi ni pale askari hao wanapovaa ki-ninja ili wasionekane nyuso zao na kuwachukua baadhi ya wananchi majumbani kwao usiku wa manane na kuwapiga na kuwatesa  kisha kuwatupa mwituni wakiwa taaban.
Mheshimiwa Spika, vitendo hivi vinavyofanywa sasa Zanzibar haifai kuvinyamazia na ni lazima Serikali ya Jamhuri ya Muungano ichukue hatua madhubuti vinginevyo vinakaribisha machafuko yasiyo na ulazima-Mwanzo wa kutoweka kwa amani uanza taratibu na kama hatua zisipochukuliwa majuto yatakuwa ni mjukuu. Amani tayari imeanza kutoweka Zanzibar!!!
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwamba UKAWA utatoa mgombea Urais mmoja na kuleta matumaini ya Watanzania na wanaojidanganya kuwa tutafarakana wanaota ndoto za mchana na watasubiri sana jambo hilo la kufarakana halitatokea.

Mheshimiwa Spika, muswada huu unaoletwa na Serikali kwa ajili ya kupitishwa una lengo la kufuta Sheria ya Benki ya Posta Tanzania, Sura 301 na kuweka masharti yatakayoiwezesha benki hiyo kusajiliwa na kuwa Kampuni, na pia kuweka masharti ya mpito kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa Sheria hii inayopendekezwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Waziri aliyoyatoa katika Kamati ya Fedha, Uchumi Viwanda na Biashara ni kwamba Benki ya Posta ilikuwa inafanya kazi bila ya kukidhi matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo ni wazi Taasisi hiyo haikuwa na haina vigezo vya kuitwa Benki, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hata kama Serikali itabadili  sheria ili ikidhi kigezo cha kuitwa benki  kwa mujibu wa sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Ambacho ni kusajiliwa chini ya sheria ya makampuni Sura, 212, lakini bado kigezo cha mtaji kitaendelea kuwa ni tatizo katika kutimiza matakwa ya  sheria ya Benki na taasisi za fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umiliki wa benki hii tunaweza kusema ni kuwa taasisi hii inamilikiwa na Watanzania kwa asilimia mia moja (100%), kwa maana kwamba Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 86.4, Tanzania Zanzibar inamiliki asilimia 3.05, Shirika la Posta Tanzania  asilimia 8.23 na Posta na Simu SACCOS asilimia 2.68. Kuhusu Zanzibar Kambi Rasmi ya Upinzani inazotaarifa kwamba inakusudia kuwekeza kiasi cha shilingi 950,000,000/- ili kuongeza hisa zake na kufikia asilimia 10 kutoka asilimia 3.05 za sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo ni mtaji na mtaji unapatikana kwa wananchi kama utaratibu ulitumika kwa Serikali kupunguza hisa zake na kuwamilikisha wananchi, kabla ya kuziweka kwenye Soko la Hisa kwa sababu tahadhari kubwa ichukuliwe ili hisa hizo zikiachwa kwenye soko zisije kuchukuliwa na wageni wachache wenye fedha, na ile dhamira ya kuwa Benki ya watanzania ikatoweka na kuleta migogoro na Serikali kama ilivyofanywa na PSRC kwa makampuni mengine.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa dhati kabisa inatoa pongezi kwa utawala na bodi ya wakurugenzi ya benki ya Posta Tanzania na hasa Mtendaji wake Mkuu kwa kuweza kuiondoa benki kutoka kwenye mtaji hasi wa shilingi milioni 78  mwaka 1992 hadi kuwa na mtaji chanya wa shilingi milioni 32,142 mwaka 2014. Hii ni kazi kubwa ukitilia maana na ushindani wa mabenki uliopo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 2 cha muswada  kinachohusu tafsiri ya maneno “benki” limetolewa tafsiri kuwa ni Benki ya Posta Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema tafsiri hiyo ingeongezewa maneno kuwa ni Benki ya Posta Tanzania iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria ya Benki na Taasisi za Fdha ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza hivyo kwa kuwa toka mwanzo Benki hiyo  ilikuwa inaitwa hivyo lakini haikuwa inakidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haipingani na hoja ya  ubadilishwaji wa sheria ya uanzishwaji wa Benki ya Posta bali inasisitiza tena hitaji la mtaji, Serikali isikimbilie kutafuta wawekezaji toka nje ya nchi, madhara yake kimbilio hilo tumeliona kupitia Benki ya Biashara (NBC 1997 Ltd). Tunaamini wapo watanzania wenye fedha nyingi za kuwezesha kutimiza sharti la mtaji kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 6 cha muswada kinahusu kuhamisha wafanyakazi waliokuwa watumishi wa Benki ya posta  na kuwa watumishi katika kampuni mpya. Jambo hili limeleta mgogoro sana na watanzania wengi ambao wana kesi zao mahakama za kazi kwa kiasi kikubwa ni kutokana na kampuni kubadilisha muundo wake. Ni maoni ya Kambi  Rasmi ya Upinzani kwamba Serikali ihakikishe na kusimamia maslahi ya watumishi, pamoja na  muswada huu wa sheria umetambua suala hilo ingekuwa ni vyema muswada ukaweka kifungu cha adhabu pale utawala wa benki utakapokiuka matakwa ya kifungu hiki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kutoa changamoto kwa watendaji wakuu wa mabenki yetu hasa (NMB, NBC, Dar es Salaam Community Commercial Bank, DTB, Akiba Commercial Bank  na sasa TPB n.k) kwa nini hasa hazijitanui hadi nchi za jirani hata kama sio zaidi ya Bara letu la Afrika?
Mheshimiwa Spika, tulitarajia NMB kwa kuwa inamilikiwa na Waholanzi kwa asilimia kubwa kuwa itafungua tawi lake Uholanzi na katika Mataifa mengine ya Ulaya, lakini imekuwa ni kinyume badala yake wanachota faida ya hapa na kupeleka nje. Tusaidieni kueleza tatizo liko wapi? Kama wenzetu wa Kenya mabenki yao yanajaa Tanzania mabenki yetu kwanini hayana matawi Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Zimbabwe, DRC n.k.
Je, ni kweli tumekosa ubunifu na uthubutu kiasi hicho? Kama ni sheria kazi yetu kama wabunge ndio kazi tunayotakiwa kuifanya ili kuleta ustawi katika sekta ambazo sheria zinawazuia.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani,
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.

………………………
Mohamed Habib J. Mnyaa (Mb)
K.n.y Msemaji Mkuu-Kambi Rasmi ya Upinzani, Wizara ya Fedha
29.06.2015


No comments: