Friday, November 30, 2012

HISTORIA YAANDIKWA PALESTINA YAIBUKA KIDEDEA




Na Mwandishi Maalum

 Palestina  jana ( alhamisi) imeibuka kidedea baada ya Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa,   kuweka historia      kwa  kupiga kura  Azimio lililoipandisha  hadhi   ya kutambuliwa kama Nchi Muangalizi  asiye Mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Azimio  hilo  lilipitishwa kwa kura 138 za ndiyo ,  kura tisa za hapana   na 41 za kutofungamana na upande  wowote. Kati ya nchi zilizopiga  kura ya  hapana na ambazo zilitegemewa ni Marekani, Israel na Canada huku  Ujerumani na Uingereza zikipiga kura ya kutofungamana na  upande wowote

Ukumbi Mkuu wa  Mikutano wa Baraza hilo ulifurika wajumbe wa  katika tukio hilo la kihistoria  lililokuwa na sura ya mchuano mkali wa mpira wa miguu ambapo kila upande ulikuwa ukijitahidi  kushangilia kwa nguvu kila msemaji wa upade fulani aliposimama kujenga hoja ya kutaka  Azimio liungwe  mkono au akijenga hoja ya kupinga  Azimio  hilo.

Azimio hilo limeungwa mkono na mataifa mengi kutoka pande zote yaani mataifa yale makubwa  kama vile Ufaransa,   China,  na Urusi nchi ambazo ni  wajumbe wa kudumu wa  Baraza   Kuu la Usalama.  Zikiwamo pia nchi nyingi  za  Jumuiya ya Ulaya,  Afrika,Asia na Visiwa vya Karibian

Tukio hilo  pia lilishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye alisema, kura ya kupitisha azimio hilo ilikuwa ikisisitiza umuhimu wa kutoa msukumo mpya wa kuanza  mazungumzo na akazisihi pande hizo mbili kuonyesha dhamira ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Licha ya ukweli kwamba bado Palestina ina safari ndefu ya kuweza kukubaliwa kuwa  mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa,  lakini kwa kukubaliwa kwake kuwa   na hadhi ya kuwa nchi muangalizi asiye mwanachama, kunaifungulia milango ya kujiunga na taasisi nyingine za kimataifa,  ikiwamo Mahakama ya Kimataifa  ya Makosa ya Jinai( ICC)  kama ikitaka kufanya hivyo.

 Akizungumza kabla ya kupiga kura,  Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, aliwataka  wajumbe wa Baraza hilo kuchukua hatua  muhimu ya kurekebisha dhuluma ambayo wametendewa wananchi wa palestina kwa muda mrefu.

Kwamba alikuwa anaitaka jumuiya ya kimataifa   kuliunga  mkono azimio hilo na hivyo  kupeleka ujumbe wa matumaini kwa wananchi wa Palestina ambao amewaelezea kama walioteseka kwa muda mrefu na waliokuwa wakielekea kukata tamaa.

 Katika hotuba yake iliyokuwa ikikatishwa mara kwa mara  kwa makofi na miluzi kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo. Kiongozi huyo wa Palestina, akabainisha kwamba walikuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona mazungumzo ya kutafuta amani kati yake na  Israeli ni kama vile yalikuwa yamekufa.

Hata  hivyo akasisitiza kwamba wamefikia hatua hiyo ya kupita Baraza Kuu  kuomba kupandishwa hadhi na kutambuliwa  kuwa nchi muangalizi asiye mwanachama  hasa baada ya ombi lao kupitia  Baraza  Kuu la Usalama kutofanyiwa  kazi.

 Lakini pia wamechukua hatua hiyo kama kielelezo cha kuthamini amani na haki yao ya msingi kama raia wengine ya  kuwa na uhuru wa  si tu  kuwa na taifa lao linalotambuliwa  bali pia haki na fursa ya kujiamulia mambo yao wenyewe.

“ Hatukuja  hapa kutaka kufuta uhalali wa  taifa fulani yaani Israeli, lakini tuko hapa kutafuta uhalali wa taifa jingine yaani Palestina,kwamba lazima sasa iijipatie uhuru wake” akasema Mahmoud Abbas

 Na kuongeza “ Tunawaomba leo hii mtupatie cheti chetu cha kuzaliwa”. Akasama Abbas na kuongeza kwamba  uamuzi huo hauna maana kwamba wanaachana na mchakato wa kurejea kwenye meza ya mazugumzo. Wala haukuwa na nia ya kutaka

Azimio la kuipandisha hadhi  Palestina limepigiwa kura katika  tarehe ( Novemba 29) ambayo  Baraza hilo lilikuwa likiadhimisha miaka 65 tangu lililopitisha azimio namba 181  lililoigawa  Palestina kuwa mataifa mawili lile la  Kiyahudi na  la Kiarabu.

Aidha Tarehe hiyo pia huadhimishwa siku ya kimataifa ya mshikamano na wananchi wa Palestina. Siku ambayo ilipitishwa mwaka 1977

Kwa upande wake  Balozi wa  Israeli  katika Umoja wa Mataifa, Ron Prosor  yenyewe imesema   nchi yake haikubaliani na azimio hilo na kwamba Palestine ilikuwa inafanya kosa kubwa na itakuja kujuta hapo baaaye.

Aidha Israel inasema haliitambui  Azimio hilo kwa sababu lilikuwa limeegemea upande mmoja na lilikuwa haliitambua taifa la  Kiyahudi.

Mjumbe  huyo wa Israeli akiongea kwa kejeli  alieleza baya kwamba,  azimio hilo haliwezi kwa namna yoyote ile kuleta amani bali   lilikuwa linarejesha nyuma mchakato wote wa kuleta amani, na kwamba yenyewe  ilikuwa inamini katika majadiliano badala ya njia za mkato mkato kama iliyofanya Palestina hiyo jana.

Nayo Marekani  kupitia Balozi wake Susan Rice    imeeleza bayana kwamba haikubaliani na azimio hilo ambalo kwao ilikuwa  ni kama kupoteza muda.

Hata  pamoja na kukandia na kuzikejeli  nchi zilizopiga kura ya kuunga mkono azimio hiyo, Marekani inasema itaendelea na juhudi zake za  kuhakikisha kwamba  mazungumzo ya kutafuta  suluhu ya kudumu kati ya pande hizo mbili yanaendelea.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ilikuwa ni kati ya nchi zilizopiga kura ya kuunga mkono azimio hilo, na Balozi  Tuvako Manongi alielezea ni kwa nini Tanzania iliamua kupiga kura ya ndiyo.

Baadhi ya sababu alizotoa ni kwamba Tanzania  ilishaitambua Palestina kama nchi huru tangu mwaka 1961 na imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo kwa miaka mingi.

Aidha akasema  kwa kupishwa kwa azimio hilo jumuia ya kimataifa ilikuwa inalitambua taifa  huru la wapalestina kama vile ilivyoitambua Israel na kwa   Tanzania  mataifa yote mawili yana uhalali wake.

Akaongeza pia kwamba Tanzania inaamini   Palestina ilikuwa na  kila sababu ya  siyo tu kutambuliwa lakini pia  kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake.

Akasisitiza kuwa Tanzania inaamini katika makubaliano na majadiliano yanayolenga  kufika suluhu ya   kuwa na mataifa mawili yakiishi sambamba na kwa amani kulingana na makubaliano ya mwaka 1947.

No comments: