Tuesday, September 19, 2017

TUME YA TAIFA YA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI(NLUPC) YATOA TATHIMINI YA UTAFITI WALIOFANYA KORIDO YA MNGETA NA UKANDA WA UDZUNGWA-MGOMBELA-SELOUS,KILOMBERO-MOROGORO

 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Dkt. Stephen Nindi (aliyesimama)akitoa maneno ya utangulizi kwa wadau wa Korido ya Mngeta na ukanda wa Magombela-Selous-Udzungwa wilayani Kilombero juu ya utafiti uliofanywa na wataalam kutoka Tume hiyo wakishirikiana na Asasi ya kiraia ya African Wildlife Foundation uliolenga maeneo ya uhifadhi wa Mazingira,Matumizi bora ya Ardhi, Hati miliki za Kimira na Bioanuai katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous, iliyofanyika Wilayani Kilombero.
 Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero (DAS)  Mh.Robert Selasela(aliyesimama) akifungua mkutano huo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kilombero uliohusu uhifadhi wa Mazingira,Matumizi bora ya Ardhi, Hati miliki za Kimira na Bioanuai katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous
Bw. Eugine Cylilo mtaalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi akitoa tathimini ya tafiti iliyofanywa na wataalamu kutoka Tume wakishirikiana na African Wildlife Foundation(AWF) ambayo ilionesha hali halisi ya usimamizi wa mipango ya Ardhi katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous juu ya,utunzaji wa Mazingira na Bioanuai,Mipango ya matumizi ya Ardhi na hati miliki za kimila na migogoro ya ardhi.
 Wadau wakimsikiliza Bw. Eugine Cylilo mtaalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi akiwasilisha utafiti huo.
 Bi. Jane Mkinga Afisa mradi wa jumuiko la maliasili Tanzania akichangia maswala juu ya maliasili
 Diwani wa kata ya Mngeta Mh. Flora Kigawa akitaka kupata ufafanuzi  wa changamoto za kutatua migogoro kati ya vijiji na pia kutaka kufahamu idadi ya wanawake wangapi wanamiliki ardhi katika wilayani Kilombero.
 Diwani wa Kata ya Chita Mh. Chelele John akiuliza maswala mbalimbali yahusuyo Ardhi.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bi. Albina Burra akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyoulizwa na wadau kuhusu utunzaji wa Mazingira na Bioanuai,Mipango ya matumizi ya Ardhi na hati miliki za kimila na migogoro ya ardhi.
 Bw. Pastor Magingi Meneja wa Programu wa  asasi yakiraia ya African Wildlife Foundation akieleza namna walivyoshirikiana  NLUPC katika utafiti wa uhifadhi wa Mazingira,Matumizi bora ya Ardhi, Hati miliki za Kimira na Bioanuai katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous
 Muwezeshaji wa Mkutano huo Bw. Geofrey Siima akiendelea kutoa Muongozo wakati wa warsha hiyo.
 Afisa Miradi kutoka asasi ya Kiraia ya Solidardad Bi. Maria Sengelela akitoa maelezo ya namna wanavyoshirikiana na NLUPC katika swala zima la matumizi bora ya Ardhi.
Afisa Sheria wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi Bi. Devotha Salukele akijibu Maswala mbali mbali yahusuyo sheria yaliyoulizwa na wananchi kuhusu Ardhi.
Afisa Ardhi Mteule kutoka Wilaya  Kilombero Bi. Syabumi Mwaipopo akifafanua na  kujibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wadau wakati wa mkutano huo.
 Afisa Mipango wa Wilaya ya Kilombero Bw. Ludwing Ngakoka akizungumza jambo wakati wa Mkutano huo
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mh. David Lugazio akitoa neno la Shukurani baada ya Mkutano huo kumalizika.
Wajumbe mbalimbali wakiendelea kufuatilia mkutano huo
Picha ya pamoja 


Katika kuhakikisha kuwa kuna mipango na matumizi bora ya ardhi nchini Tanzania, Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya African Wildlife Foundation (AWF) walifanya utafiti wa uhifadhi wa Mazingira,Matumizi bora ya Ardhi, Hati miliki za Kimila na Bioanuai katika korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous Wilayani Kilombero.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha utafiti huo kwa Madiwani, Watendaji Wilaya, Tarafa na Kata, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya matumizi ya Ardhi (NLUPC) Dkt. Stephen Nindi alisema kuwa Tume ilifanya utafiti katika ushoroba wa Mngeta pamoja na ukanda wa Udzungwa-Magombela-Selous lengo likiwa ni kuangalia mambo mbalimbali yanayohusu matumizi bora ya Ardhi, umiliki wa ardhi, uhifadhi ya mazingira na Bioanoai katika maeneo hayo.

Mkurugenzi Mkuu alidokeza kuwa Wilaya ya Kilombero ni moja ya Wilaya tajiri katika nchi ya Tanzania ambayo ina ardhi yenye rotuba kubwa inayofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali pamoja na uoto wa aina mbalimbali “Kuna matumizi ya aina mbalimbali ya ardhi katika Wilaya hii, tuna wakulima, wawekezaji wakubwa katika kilimo, wawekezaji wakubwa katika misitu, hifadhi ya wanyama pori, kilomo cha kati na kilimo cha wakulima wadogo wadogo, wafugaji, wavuvi, wafanya biashara ambao kwa umoja wanatengeneza ubia mbalimbali katika matumizi ya Ardhi” alisema Dkt. Nindi.

Aliongeza kuwa lengo la utafiti huu ilikuwa kuangalia wadau mbalimbali katika utumiaji, upangaji na usimamizi wa ardhi wanatekelezaje, kuangalia changamoto za mipango ya matumizi ya Ardhi, umiliki wa ardhi,uhifadhi wa mazingira na Bioanoai.

“Tupo hapa kwa ajili ya kuwasilisha utafiti wetu kwamba namna gani mambo haya yanafanyika shughuli hizi za uhifadhi wa mazingira na Bioanoai, Shughuli za upangaji na matumizi ya Ardhi, umiliki wa Adhi pamoja na utekelezaji wake na usimamizi zinavyofanyika katika kanda hizi mbili” alisema Dkt. Nindi.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mtaalamu wa mazingira kutoka Tume bwana Eugen Cyrilo, alibainisha changamoto kadhaa matumizi ya ardhi, umiliki pamoja na uhifadhi wa mazingira. “Changamoto kubwa iliyobainika katika utafiti huu, ni utekelezaji wa maipango ya matumizi ya ardhi. Vijiji vingi tulivyopitia vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi, ila kwa kuwa hakuna usimamizi wa mipango hiyo kwa ngazi ya vijiji, kunakuwa hakuna utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi waliojitengea” alieleza bwana Cyrilo.

Aidha, katika upande wa mazingira, ilibainika kuwa kumekuwa usimamizi usioridhisha hasa kwenye misitu na vyanzo vya maji kwa baadhi wanavijiji wenyewe au watu kutoka nje ya vijiji kuvamia na kuweka makazi kwenye misitu ikiwa pamoja na kukata miti bila utaratibu. “Kwenye baadhi ya maeneo, kumekuwa na uvamizi wa misitu ambapo hapo awali ilikuwa imetengwa kwa ajili ya uhifadhi, na sehemu zingine tulikuta wanavijiji wakifanya shughuli ambazo si rafiki kwa mazingira pembezoni mwa mito, hii ni tishio kubwa katika utunzaji wa mazingira” alisema bwana Cyrilo.

Akichangia katika matokeo ya utafiti huo, Meneja wa Programu kutoka AWF bwana Pastor Magingi aliwasihi uongozi wa Wilaya kuja na suluhisho la kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi ili kufanya kazi nguvu kubwa inayofanywa na na Tume, Wadau pamoja na Halmashauri yenyewe isipotee bure.

Hatua hii iliwapelekea Madiwani wa Kata zilizohusika kwenye utafiti huu kupendekeza kuwapo kwa mtaalamu wa Wilaya atakayehusika moja moja na kusimamia utekelezakji  wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya ili kutoa ripoti ya mara kwa mara juu ya usimamaizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuwa endelevu na yenye manufaa kwa wananchi.

Utafiti huo ulihusisha Kata nne za ukanda wa Udzungwa-Magombera-Selous, ambazo ni Msolwa Stesheni, Mkula, Mang'ula B na Sanje pia kulikuwa na vijiji nane vya Msolwa Stesheni, Mkula, Sonjo, Msufini,Katurukila, Kanyenja, Magombera na Sanje. Aidha katika korido ya Mngeta utafiti huo ulihusisha kata sita za Namawala, Igima, Mbingu, Mngeta, Chita na Mofu pamoja na Vijiji  vya Mofu, Ihenga, Kisegese, Vigaeni, Makutano, Igima, Mbingu, Njage, Mngeta, Mchombe na Lukolongo.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA-ULINZI UIMARISHWE KWENYE MAENEO YA VIWANDA NA UWEKEZAJIWaziri mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,wakati alipowasili katika kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Pichandege Kibaha Mjini.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkurugenzi wa viwanda vya kutengeneza sabuni cha KEDS Pichandege Kibaha Mjini ambae pia ni mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze,Jack Feng.Picha na Mwamvua MwinyiNa Mwamvua Mwinyi,Pwani

WAZIRI mkuu,Kassim Majaliwa amezitaka serikali za vijiji na ngazi nyingine mkoani Pwani,kujikita kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili kulinda mali na usalama wa wawekezaji na watanzania kijumla.

Amesema haijajulikana hadi sasa nia na dhamira ya watu wasiojulikana wanaojihusisha kupoteza maisha ya watu ,na ni hatari endapo watajiingiza katika maeneo ya uwekezaji kwani hakuna mwenye uhakika wa azma yao.

Aidha Majaliwa ,ametoa wiki mbili kwa waziri wa maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa WAMI ,ili kutoa utaratibu na kama sheria inaruhusu kuvunja mkataba ikiwa mkandarasi ameshafikia kiwango cha asimilia 50 ya utekelezaji.

Waziri huyo ,pia ameziagiza halmashauri nchini kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya zimamoto yatakayosaidia kudhibiti majanga ya moto yanapotokea hususan kwenye maeneo ya uzalishaji na viwanda.

Katika hatua nyingine amelitaka shirika la umeme Tanesco,Dawasco kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya umeme na maji katika maeneo yenye uwekezaji ili kuvutia wawekezaji.

Alitoa rai hiyo,wakati wa ziara yake ya siku moja ,aliyoifanya mkoani Pwani kutembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Kibaha,na cha kutengeneza vigae Twyford Ceramics Ltd/Pingo,Chalinze ,Bagamoyo.

Majaliwa ,alieleza kuwa ni lazima raia mmoja mmoja na jukumu la kila mmoja kusimamia kulinda nchi kuanzia maeneo wanayoishi .

Alisema serikali imejipanga kuendelea kusimamia amani na utulivu,ambapo amewataka wananchi waiunge mkono serikali kupambana na wahalifu wasio na nia njema na serikali.

“Hatuna uhakika kwa watu hawa wanaofanya vitendo vya ovyo,watanzan ia waungane na serikali,kupambana ili wasije kuingia kwa wawekezaji na kupoteza ndoto za serikali za kupata wawekezaji “alisema Majaliwa.

Akizungumzia tatizo la uhaba wa maji ,alisema mradi wa WAMI ulikuwa ukamilike tangu mwezi July mwaka huu.

Alisema alitembelea mradi huo mwezi juni mwaka huu ukiwa chini ya asilimia 38 na kusema mkandarasi akiendelea kusuasua watamfukuza na kutoa agizo ikifika mwezi huu wafikie asimilia 80.

“Nilitaka kuja mwezi huu lakini nikaambiwa speed ni ndogo na bado hali hairidhishi,na mkandarasi hajamaliza”mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amekuwa akiuliza juu ya kukwama kwa mradi huo” ;”Nimetoa wiki mbili kwa waziri aangalie dhamana ya kampuni kwenye ubalozi wao wa India na kuangalia sheria namna ya kufanya ama kukamilisha mradi kwa muda mfupi uliobaki”alifafanua.

Kuhusu nishati ya umeme Majaliwa,alisema serikali ipo mbioni kutekeleza mradi mkubwa wa umeme stiegler’s gorge katika chanzo cha mto Rufiji, utakaozalisha megawatts 2,100 zitakazoondoa kama si kumaliza upungufu wa umeme uliopo.

Aliitaka halmashauri ya Chalinze,ijipange kwa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji.

Kuhusu suala la zimamoto ,Majaliwa alisema mkoa huo kwasasa una viwanda vikubwa hivyo wakati serikali ikipokea changamoto ya uhaba wa vifaa na magari ya zimamoto ,halmashauri ijipange kupitia bajeti zao.

“Viwanda hivi ni vikubwa vinajengwa ,kiwanda hiki cha KEDS kina jengo hilo hapo lenye urefu wa mita 30 juu,tuombe mungu moto usitokee ,unawezaje kuzima moto kwa maji ya kwenye ndoo ,ipo haja ya kuangalia namna ya kutatua changamoto hii”

“Dar es salaam ambako ni mji wa kibiashara serikali itasaidia katika kununua mitambo ya kusaidia kuzima moto kutegemea ukubwa wa majengo yaliyopo”aliongeza Majaliwa.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara,alitoa rai kwa halmashauri ya Mji wa Kibaha kuboresha barabara zilizopita mitaani na kuhakikisha mitaa yote iwe na barabara bora kwa kufumua zisizofaa na kuchonga barabara zenye viwango.

Pamoja na hayo ,Majaliwa alibainisha uwekezaji kama huu unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda ambapo itaongeza pato la nchi na itazalisha ajira kwa wingi.

Aliwasihi vijana ambao tayari wana ajira kwenye viwanda hivyo kutumia nafasi walizozipata kwa kuchapa kazi .

Majaliwa aliwaomba vijana hao kuchapa kazi na kuwathibitishia wawekezaji kuwa watanzania ni wachapazi na wana uwezo wa kufanyakazi viwandani na hakuna haja ya kuleta watumishi nje ya nchi.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,alimwambia waziri mkuu ,kwamba mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara isiyo ya kuridhisha kwa wawekezaji.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa nishati ya umeme isiyokidhi mahitaji kwani kwasasa mahitaji ni megawatts 73.2 na uliopo ni megawatts 40 ambao bado hautoshelezi.

Mhandisi Ndikilo,alieleza tatizo la uhaba wa vifaa,vitendea kazi na magari kwa idara ya zimamoto na kuhofia endapo janga la moto likitokea kushindwa kuzima moto kwa wakati na kusababisha athari kubwa.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ,alilalamikia uzembe na uvivu uliokubuhu katika utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze (CHALIWASA).

Alielezea kuwa,tatizo la maji limedumu kwa takribani miaka 13 sasa hali inayosababisha adha kwa wawekezaji na wananchi kijumla.

Ridhiwani alisema ,haridhishwi na mwenendo wa mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi huo kutokana na kasi yake kuwa ni ndogo na haiendani na maagizo aliyoyatoa waziri mkuu hapo awali.

Akiwa kiwanda cha KEDS ,mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka ,alimuomba Majaliwa kuangalia kwa jicho la tatu kero ya miundombinu isiyo rafiki kwa wawekezaji.

Koka alisema wawekezaji wengi wanakimbilia kuwekeza mji wa Kibaha na mji huo upo usoni mwa barabara kuu ya Morogoro-Dar es salaam lakini bado kuna tatizo la barabara mbovu.

Wakati huo huo ,mkurugenzi mkuu wa kiwanda cha KEDS na Twyford ,Jack Feng alisema asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka hapa nchini .

Alisema katika kiwanda cha KEDS wameshaajiri watu 200 huku wakitarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 katika kiwanda hicho .

‘Ndani ya ujenzi huu kuna kiwanda kingine kikubwa ambacho tutazalisha bidhaa ya pempars na kiwanda kingine tutatengeneza misumali”alieleza Feng.

Alisema hatua ya ujenzi ni nzuri imefikia asilimia 90 na wanategemea kuanza uzalishaji mwezi ujao,na utagharimu dola mil.200 hadi utakapokamilika.

Feng alifafanua,kwenye kiwanda cha Twyford watarajia kuajiri wafanyakazi 4,000 hadi 6,000 mara watakapoanza kuzalisha mwezi Nov mwaka huu,sasa kuna wafanyakazi 1,200.

Mkurugenzi huyo ,alieleza gharama ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Twyford ni dola mil. 56 sawa na bilioni 120 na watauza vigae ndani ya nchi hadi nje ya nchi Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi.

PROF. MAGHEMBE ATOA SIKU 40 KWA WALIOLIMA NDANI YA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA WAONDOKE KWA HIARI

Na HAMZA TEMBA - WMU
-----------------------------------------------------------
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuhakikisha kuwa wananchi wote waliolima ndani ya eneo la hifadhi hiyo kinyume cha sheria wanaondoa mazao yao pamoja na kusitisha kabisa shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi hiyo.  

Prof. Maghembe ametoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na hifadhi hiyo ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.

"Naagiza, kuanzia leo ni marufuku mtu yeyote kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka", alisisitiza Prof. Maghembe baada ya kukagua eneo hilo.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri Maghembe, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga alisema eneo hilo ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na mgogoro tangu mwaka 1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung'wado kuvamia eneo hilo huku wakitoa hoja kadhaa ikiwemo madai kuwa shamba hilo ni maeneo yao ya asili waliyokuwa wakimiliki tangu zamani.

Alisema hoja nyingine wanazozitoa ni kuwa walipewa mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka 1975 na 1976, Aidha, hoja nyingine ni kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na kwamba TANAPA pia haina hati miliki ya mashamba hayo.

Ngada alisema hoja zote hizo zilikinzana na ukweli ya kwamba shamba hilo lilimilikishwa kwa TANAPA tangu mwaka 1980 baada ya kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kufuatia muwekezaji wa awali, James Preston Mallory kushindwa kuliendeleza na hivyo kufutiwa hati miliki na Mhe. Rais mnamo mwaka 1979.

“Wadau mbalimbali waliomba umiliki wake ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Halmashauri ya Kijiji cha Olkung'wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha ikaishauri Serikali mashamba hayo yamilikiwe na TANAPA na hivyo tukaandikiwa barua rasmi ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa” alisema Ndaga.

Alisema TANAPA ilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 966 kwa lengo la kupanua hifadhi ya Taifa ya Arusha ambapo baada kupewa shamba hilo, iliagizwa kulipa fidia ya mali zilizokuwepo, mwaka 1983 tathmini ikafanyika na malipo yakalipwa Serikalini hatimaye TANAPA ikapewa barua ya kumiliki ardhi mwaka 1988. Alisema kwa upande wa Kijiji hicho cha Olkung'wado hakuna nyaraka yeyote inayoonesha shamba hilo kupewa kijiji hicho. 

Mhifadhi huyo alisema baada ya mgogoro wa muda mrefu, wataalam wa TANAPA walifanya survey katika shamba hilo ili kubaini maeneo yaliyo na shughuli nyingi za kibinadamu na yale yenye umuhimu zaidi kiikolojia, mapendekezo yalitolewa kuwa maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu yaachwe kwa wananchi na yale yenye umuhimu kiikolojia yaendelee kuhifadhiwa, Bodi ya TANAPA iliridhia ekari 366 zipewe wananchi na ekari 600 ziendelee kuhifadhiwa.

“Baada ya kikao cha wadau wa uhifadhi kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru tarehe 11 Mei, 2017 ambacho kilijumuisha Madiwani, mwakilishi wa Mbunge, katibu tarafa, watendaji wa kata, wenyeviti na watendaji wa vijiji, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na wataalam wa halmashauri, ilifikiwa maazimio ambapo wajumbe waliridhia maamuzi ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kuwapa wananchi ekari 366 ya shamba hilo na kubakiwa na ekari 600” alisema Ndaga.

Aliongeza “Kikao hicho pia kiliridhia TANAPA kuweka vigingi vya mpaka katika shamba hilo ambapo tarehe 14 Mei, mwaka huu, 2017 zoezi hilo lilianza na jumla ya vigingi 26 viliwekwa”.

Alisema hata hivyo kumekuwepo na taarifa kuwa baadhi ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella walifungua kesi mahakamani wakidai wakidai kuwa kijiji cha Olkung'wado kimenyang'anywa ardhi yao na TANAPA, hata hivyo Serikali hiyo ya Kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa kesi hiyo wakidai imefunguliwa na mtu binafsi na sio Serikali ya Kijiji hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi alimuhakikishia Waziri Maghembe kuwa maagizo yote aliyoyatoa ya kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi na atapewa mrejesho wa utekelezaji wake.

Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilianzishwa mwaka 1960 wakati huo ikiitwa Ngurdoto na ina ukubwa wa kilomita za mraba 322. Hifadhi hiyo ni maarufu kwa utalii wa magari, kutembea kwa miguu, kupanda milima (mlima Meru), utalii wa farasi, mitumbwi ya kuogelea, baiskeli na wa utalii wa kutumia farasi. Katika mwaka wa fedha uliopita 2016/2017 hifadhi hiyo ilivunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 12 ambapo ilikusanya Shilingi bil. 5.4.
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiingia kwenye ofisi kuu ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana Mkoani Arusha katika ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga alipowasili katika ofisi kuu ya hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi.
Prof. Maghembe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi (kushoto) akizungumza kutambulisha viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha ambapo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) na wajumbe wa kikao hicho wakifuatilia taarifa kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Arusha ambayo iliwasilishwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiongea na viongozi wa TANAPA kuhusu eneo lililolimwa na wananchi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha kinyume cha sheria wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi, aliagiza wananchi hao waondolewe ndani ya siku 40. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi na Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akisikiliza ufafanuzi wa jambo kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Baadhi ya wanyamapori (Twiga na Pundamilia) wakionekana wakijivinjari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 

SERIKALI ITAHAKIKISHA MIRADI YA UMEME, MBAGALA, KURASINI NA KIGAMBONI INAKAMILIKA-DKT. KALEMANI

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, (wakwanza kulia), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, (wakwanza kushoto), na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Khalid James, (watatu kushoto), wakimsikiliza Meneja Mradi wa TEDAP, Mhandisi Emmanuel Manirabona, (aliyenyoosha mkono), wakati Naibu Waziri na uongpozi wa TANESCO, ulipotembelea mradi wa TEDAP wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam, Septemba 18, 2017. Mradi huo unahusu upanuzi na uendelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme wa 132kv.

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), imeahidi kusimamia miradi ya umeme Kituo cha Tipper-Kigamboni,  Mbagala na Kurasini ili kuhakikisha inakamilika kwa haraka na kwa wakati na hatimaye wananchi wa maeneo hayo wanaondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, mwishoni mwa ziara yake ya kufuatilia uboreshaji wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kufua na kusambaza umeme huko Kimbiji  wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Septemba 18, 2017.

Waziri pia amekagua ujenzi wa mradi wa maendeleo ya upanuzi na upatikanaji nishati (TEDAP), wa kusafirisha umeme wa 132kv ulioko Gongolamboto nje kidogo ya jiji.

“Wananchi wanataka umeme, hawahitaji kujua  nguzo za umeme zimepatikana wapi, au upembuzi yakinifu utakamilika lini, nimeagiza baada ya siku tano kuanzia leo (Septemba 18), fanyeni kazi usiku na mchana walau vituo viwili vya kupoza na kusambaza umeme viwe vimekamilika ili wananchi wa Mbagala na Kigamboni wapate umeme wa kutosha.” Alisema Dkt. 

Kalemani mbele ya Mbunge wa Kigamboni Dkt. Faustine Ndungulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi, Dkt. Tito Mwinuka na viongizi wengine wa Tanesco.

Dkt. Kalemani alisema, miradi hiyo imechukua muda mrefu, na kwamba hakuna muda zaidi utakaoongezwa kuikamilisha.Serikali kupitia TANESCO, inatekeleza miradi mitano ya kuongeza kiasi cha umeme kwenye maeneo ya Mbagala na maeeno kadhaa ya wilaya ya Temeke, Kurasini na Kigamboni ili kukabiliana na ongezeko la kasi la watu na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Aidha Naibu Waziri aliipongeza TANESCO, kwa kutekeleza agizo lake la kuhakikisha wakazi 3,500 wa Kigamboni waliolipia ili kuunganishiwa umeme, wawe wameunganishiwa ifikapo Septemba 15, 2017 ikiwa ni pamoja na kupeleka nguzo za umeme zaidi ya 1,000 maagizo ambayo yametekelezwa.

Hata hivyo naibu Waziri alimueleza Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni na Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa tiba mahsusi ya upungufu wa umeme kwenye wilaya hiyo ni kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme cha Kimbiji.

“Tiba kubwa ya matatizo ya umeme kwa watu wa Kigamboni, na Mbagala ni hapa Kimbiji(kituo kipya), vile vituo vingine vitapunguza tu matatizo lakini naomba Mheshimiwa Mbunge, uwafikishie ujumbe wananchi kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayo dhamira ya kweli ya kuhakikisha inawapatia umeme wa uhakika sio tu wananchi wa Kigamboni bali watanzania wote kwa ujumla.” Alifafanua Dkt. Kalemani.

Naibu Waziri ameshuhudia hatua mbalimbali za ukamilishaji wa miradi hiyo zikiwa zimefikiwa ambapo katika kituo maeneo yote aliyotembelea.
Kuhusu ujenzi wa kituo kipya cha Kimbiji, Dkt. Kalemani amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANSCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, kuwaleta mafundi wa TANESCO wealiotekeleza kwa muda mfupi ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza na ksuambaza umeme kule Mtwara ili waje kuongeza nguvu.
Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile, (kushoto), akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ambaye alifuatana naye kwenye ziara hiyo.
Sakafu ya kufungia transfoma mpya ya umeme wa 15mva kituo cha Tipper-Kigamboni, ikijengwa Septemba 18, 2017
Mshine mpya kwenye kituo cha Mbagala
Kituo cha Kurasini ambacho nacho kitakuwa tayari baada ya siku tano.
Dkt. Kalemani, (katikati), Dkt. Ndungulile (wapili kushoto) na Dkt. Mwinuka, (wakwanza kushoto), wakiwa na Meneja wa Mradi wa TADEP, Mhandisi Emmanuel Manirabona, (kulia), baada ya kujionea moja ya mashine mpya ikiwa bado imefunikwa ili kuzuia vumbi kwenye kituo cha Kurasini.
Fundi akiwa kazini kwenye kituo cha Kurasini.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani, na Mbunge wa Kigamboni Dkt. Ndungulile, wakiwa na furaha baada ya kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mbagala, ambacho ujenzi wake umekamilika
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila, akizungumza mwishoni mwa ziara ya Naibu Waziri, Dkt. Kalemani huko Kimbiji.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani na Mhandisi Khalid James.
Msafara wa Naibu Waziri ukiwa kwenye eneo la mradi wa TEDAP. Gongolombaoto.
Mkandarasi anayejenga mradi wa TEDAP, Gongolamboto, akizunguzma.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, anayeshughulikia usambazaji umeme na huduma kwa wateja mama Joyce Ngahyoma, akielezea hatua zilizochukuliwa na TANESCO katika kuhakikisha wateja 3,500 wa TANESCO Kigamboni waliolipia gharama za kuunganishiwa umeme, wanapatiwa huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa nguzo zaidi ya 1,000 kwenye eneo la Kigamboni. Anayemsikiliza ni Naibu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani.
Kituo cha Mbagala
Dkt. Kalemani, (kushoto), akimsikiliza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula akielezea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Tipper-Kigamboni.
Dkt. Kalemani, (wapili kushoto), akizungumza jambo na Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, walipowasili eneo la Kimbiji ambako kunatarajiwa kujengwa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme kitakachohudumia wakazi wa Kigamboni, Kurasini na Mbagala. Wakwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO nayeshughulikia Miradi, Mhandisi Khalid James.